Benki ya Dunia imesema kuwa uhusiano baina yake na Tanzania ni imara na kuihakikishia nchi hiyo ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimaendeleo.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, – Mara Marwick ameyasema hayo katika ofisi ndogo za wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa wizara hiyo Profesa Palamagamba Kabudi.
Marwick amesema kuwa Benki ya Dunia iko tayari kuendelea kuunga mkono kwa njia ya ufadhili au mikopo, miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Tanzania.
“Tuna uhusiano mzuri katika miradi na uwekezaji ambapo tunaiwezesha Serikali katika maeneo mbalimbali, pia tunafanya kazi pamoja katika masuala muhimu kama vile uchambuzi wa sera za maendeleo, hii inaashiria kuwa Benki ya Dunia itaendeleza ushirikiano huu katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na mahusiano imara pamoja na maendeleo endelevu,” amesema Mkurugenzi Mkazi huyo wa Benki ya Dunia.
Kwa upande wake Profesa Kabudi amesema kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano na Benki ya Dunia na kuwataka Watanzania kupuuza uzushi na uvumi unaosambazwa katika mitandao ya kijamii kuhusu mahusiano baina ya Tanzania na Benki hiyo na badala yake wasubiri taarifa rasmi kutoka Serikalini na Benki hiyo.
“Uhusiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia ni imara na unaendelea vizuri, na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia ametuhakikishia kwamba katika kipindi hiki ambacho yeye ni Mkurugenzi hapa atauendeleza uhusiano huo huo, mengi yanasemwa lakini mengi hayana ukweli na wakati mwingine si busara kwa kila yanayosemwa kuyajibu kwasababu yanaweza kuwaondoa kwenye shughuli za msingi na mkajikuta kila siku mnajibu uvumi au uzushi katika mitandao ya kijamii na mambo mengine,” amesema Profesa Kabudi.