Tanzania kuanza majaribio ya reli ya kisasa

0
837

Tanzania inakusudia kufanya majaribio rasmi ya Reli ya kisasa (SGR) kuanzia mwezi Mei mwaka huu, baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Reli hiyo mwezi Aprili.

Meneja wa mradi wa ujenzi wa reli hiyo Machibya Masanja amesema kuwa, ujenzi unakwenda kama ulivyopangwa na kwamba majaribio hayo yatafanyika kwa kipindi cha miezi mitatu kabla ya uzinduzi rasmi ambao utaruhusu kuanza usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo.

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo ya kisasa inajumuisha Kilomita 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, ambapo umekamilika kwa asilimia 72 hadi sasa.

Ujenzi huo ulitarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka 2019, lakini ulishindwa kukamilika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na kukwamisha shughuli mbalimbali.

Awamu hiyo ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo ya kisasa itakuwa na vituo Sita, ambapo vituo vya Dar es salaam na Morogoro ndivyo vitakuwa vikubwa na vingine ni Pugu, Soga, Ruvu na Ngerengere.

Ujenzi wa awamu ya Pili wa reli hiyo ya kisasa yenye urefu wa kilomita 422 kutoka Morogoro hadi Makutupora jijini Dodoma tayari umeanza na umekamilika kwa asilimia Ishirini.