Miili ya askari polisi watatu waliofariki Njombe yaagwa

0
487

Miili ya askari polisi watatu waliofariki katika ajali ya gari Februari 3 mwaka huu mkoani Njombe inaagwa leo katika viwanja vya polisi mkoani humo, ikiwa tayari kusafirishwa kwa ajili ya mazishi.

Ibada ya kuaga miili hiyo imehudhuriwa na viongozi wa serikali ya mkoa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Christopher Ole Sendeka, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri.

Wengine waliohudhuria ni wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama, askari wa vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini pamoja na wananchi wa mkoa huo.

Askari hao walifariki jana baada ya gari walilokuwa wakisafiria kwenda lindo kugongana na basi la abiria katika daraja la Mto Ruhiji mjini Njombe.

Mbali na hao, askari wengine tisa walijeruhiwa na kupelekwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa ajili ya matibabu.