Serikali ya Kenya imetangaza kuanza kwa maombolezo ya Kitaifa kufuatia kifo cha Rais wa Pili wa nchi hiyo Mzee Daniel Arap Moi.
Akitangaza kuanza kwa maombolezo hayo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema kuwa, maombolezo hayo yataendelea hadi hapo yatakapofanyika mazishi ya Kiongozi huyo, mazishi ambayo hadi sasa haijatangazwa yatafanyika lini.
Wakati wa siku zote za maombolezo, Rais Kenyatta ameagiza bendera zote nchini humo kupepea nusu mlingoti ikiwa ni ishara ya kumuenzi Mzee Moi, Kiongozi ambaye ameliongoza Taifa hilo kwa muda mrefu.
Mzee Moi amefariki dunia alfajiri ya leo katika Hospitali ya Nairobi alipokua akipatiwa matibabu, huku kukiwa na taarifa kuwa alilazwa hospitalini tangu mwezi Oktoba mwaka 2019.
Moi amekua Rais wa Kenya kuanzia Oktoba 14 mwaka 1978 hadi Disemba 30 mwaka 2002.