Kangi Lugola alilidanganya Bunge kuhusu ununuzi sare za polisi

0
1207

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka amesema kuwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alilidanganya Bunge la Tanzania kuhusu ununuzi wa sera za jeshi la polisi.

Kaboyoka ameyasema hayo leo bungeni, Dodoma wakati akisoma ripoti ya kamati hiyo baada ya kufuatilia sakata hilo, ambapo waliangalia masuala mbalimbali ikiwemo namna zabuni ya tenda hiyo ilivyopatikana, kiwango cha fedha kilichotumika na zilipotoka sare hizo.

“Kwa hiyo Kangi alilipotosha bunge kwa kuapa kwamba atavua nguo kama uniform (sare) hizo hazipo, inamaana hasomi hata taratibu,” amesema Kaboyoka.

Mwenyekiti huyo amemtaka Lugola aeleze sare hizo zilinunuliwa kutoa wapi pamoja na gharama zilizotumika ili Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atafuatilia sakata hilo, kujua kama taarifa ya sare atakayoitoa, itaendana taarifa ya sare zilizopo.

Wakati hayo yakitokea bungeni, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Mbungo amesema kuwa wamekamilisha ukusanyaji wa taarifa za awali za sakata linalomkabili Lugola, na muda si mrefu watamuhoji.

Mbali na Lugola, wengine watakaohojiwa ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Ramadhani Kailima, Mkuu wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye, na Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene.

Mbungo amesema Simbachawene atahojiwa kwa sababu ndiye aliyekabidhiwa wizara hiyo na Rais Dkt Magufuli.

Januari 23, mwaka huu Rais Dkt Magufuli alitengua uteuzi wa Kangi Lugola kutokana na kutia saini ununuzi wa vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Tsh trilioni 1.04 kutoka kampuni ya nje ya nchi bila kufuata sheria.

Rais alisema katika mchakato wa zabuni hiyo baadhi ya viongozi wa jeshi la zimamoto na uokoaji walikuwa wakikaa kwenye vikao na kulipwa posho Tsh milioni 1.8, ambapo Tsh milioni 1.2 ilikuwa ni posho ya kikao na Tsh laki 6.9 ikiwa ni posho ya safari na tarakilishi mpakato (laptop) kwa kila mmoja kila walipokutana.