Wadau watakiwa kujitokeza kuishangilia Stars

0
1948

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe  ameendelea kuwasisitiza wadau wa michezo  nchini kukata tiketi kwa ajili ya kwenda Cape Verde kuishangilia timu ya Taifa ya  mpira wa miguu -Taifa Stars ambayo itasafiri na ndege ya Dreamliner kwa ajili ya mchezo wa kufuzu kwa fainali za AFCON, mchezo utakaochezwa Oktoba 12 mwaka huu mjini Pria.

Akizungumza katika kipindi cha Meza ya Michezo kitachotangazwa na TBC I, Waziri  Mwakyembe amesema kuwa  tiketi za ndege zitauzwa kwa dola 1, 500 za Kimarekani na nyingine kwa dola 2000 za kimarekani kwa safari ya kwenda na kurudi.

Waziri  Mwakyembe amesema kuwa ili kuhakikisha safari hiyo inafanikiwa, serikali imetoa ndege hiyo ya Dreamliner ambayo itabeba wachezaji wa timu ya taifa na viongozi wake kuelekea Cape Verde kwa ajili ya mechi hiyo na kuongeza kuwa mchezo huo ni muhimu kwa Taifa Stars, hivyo nguvu ya mashabiki wa kuishangilia inahitajika.

“Kwa kweli serikali yetu imeonyesha nia kwa kutoa ndege ya kisasa ya Dreamliner yenye uwezo wa kubeba watu 250 ambapo kikosi cha wachezaji kina watu 31, hivyo wanahitajika watu zaidi ya 200 kukamilisha idadi kamili ya abiria”amesema Dkt Mwakyembe.

Ameongeza kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) limelipa dola  elfu  69 za kimarekani  kwa ajili ya kusafirisha timu hiyo, huku nafasi zilizobaki ni kwa ajili ya wadau wa michezo walio tayari kuungana na Taifa Stars kuelekea Cape Verde.

“Kitendo cha timu kushuka Cape Verde na Dreamliner tena ndege ya nyumbani tayari tumekwishapiga goli mbili, hizo zingine namuachia Amunike na benchi la ufundi waongezee” ameongeza Dkt Mwakyembe.

Mchezo wa marudiano kati ya Taifa Stars na timu ya Taifa ya Cape Verde utafanyika siku tatu baadae yani oktoba 16.

Mara ya mwisho Tanzania kucheza fainali za AFCON ilikuwa mwaka 1980.