Maeneo yaliyokumbwa na tetemeko Indonesia yafikiwa

0
2085

Vikosi vya uokoaji nchini Indonesia vimesema kuwa vimeweza kuzifikia wilaya zote nne zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi pamoja na tetemeko la chini ya bahari – Tsunami katika kisiwa cha Sulawesi.

Wafanyakazi wa vikosi hivyo wamesema kuwa misaada ya chakula, maji na mafuta ya kula inaendelea kusambazwa katika maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na tetemeko hilo.

Hata hivyo wafanyakazi hao wamesema kuwa wamekua wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kuharibika kwa miundombinu hasa ya barabara, na hivyo kuathiri kazi ya kusambaza misaada hiyo.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa zaidi ya watu laki mbili walionusurika katika tetemeko hilo wanahitaji msaada wa haraka.

Mpaka sasa zaidi ya watu elfu moja na mia tatu wamethibitika kufa kutokana na tetemeko hilo la ardhi na lile la chini ya bahari – Tsunami huku  idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka.