Rais Magufuli ateua viongozi wa bodi, TNBC na Chuo Cha Maji

0
265

Rais Dkt. John Magufuli amefanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi wanne, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa -TNBC na Mkuu wa Chuo cha Maji.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi
imeeleza kuwa uteuzi wa viongozi hao umeanza tarehe 20 Januari, 2020.

Walioteuliwa ni Prof. Maurice Mbago kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania -TEA. Prof. Mbago anashika wadhifa huo kwa kipindi cha pili, Dkt. Masatu Chiguna kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania -TAA. Dkt. Chiguna anachukua nafasi ya Prof. Ninatubu Lema ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na bodi kuvunjwa.

Halikadhalika Rais Magufuli amemteua Prof. Zacharia Mganilwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli -MSCL.
Prof. Mganilwa ni Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji -NIT.

Mariam Nkumbi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua Dkt. Godwill Wanga kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa -TNBC.

Kabla ya uteuzi huo Dkt. Wanga alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam -UDSM.

Aidha, Rais Magufuli amemteua Dkt. Adam Omar Karia kuwa mkuu wa Chuo cha Maji.