Waziri Mkuu yaagiza watoto wa kike walindwe wamalize shule

0
383

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini wasimamie ipasavyo suala la elimu, hususani kwa watoto wa kike na kuchukua hatua kwa watakaowakatisha masomo.

Agizo hilo limetolewa jana, Januari 19 wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali cha Daya kilichopo Mtambwe wilaya ya Wete, Pemba Kaskazini.

Pia watoto wakike wamepewa sauti ya kutoa taarifa za watu wanaotaka kuwakatisha masomo yao kwa viongozi wa vijiji.

“Wanafunzi wa kike hakikisha mtu yeyote atakayekugusa, kukufuatilia nenda kamshtaki kwa kiongozi wa shehiya husika. Vijana jihadharini na watoto wa shule ukikutwa naye jela miaka 30,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa serikali imedhamiria kuwalinda watoto wa kike, lengo likiwa ni kuhakikisha wanamaliza masomo yao na hatimaye waweze kujikwamua wao pamoja na familia zao.

Awali, akisoma taarifa za ujenzi wa chuo hicho, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Madina Abdallah amesema, mpaka kukamilika kwake mradi huo utagharimu jumla ya dola za kimarekani milioni 25,8 sawa na shilingi bilioni 59,6 za kitanzania.

Kati yake bilioni 54,1 zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) huku bilioni 5,5 zikitolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).