Waziri Mkuu aagiza kuzuiwa utoaji wa vibali vya kuagiza sukari

0
397

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda, Juma Hassan Reli kuzuia utoaji wa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje ya nchi hadi hapo sukari inayozalishwa na kiwanda cha sukari cha Zanzibar iishe.

Waziri Mkuu Ameyasema hayo alipotembelea kiwanda cha kuzalisha sukari cha Zanzibar kilichopo katika eneo la Mahonda, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ mkoani Kaskazini Unguja na kueleza kuwa haiwezekani kiwanda hicho pekee kinachozalisha tani 6,000 za sukari kwa mwaka kikakosa wateja wakati mahitaji ya sukari Zanzibar ni tani 36,000 kwa mwaka.

“Wizara ya Viwanda lazima mbadilike na muweke utaratibu mzuri wa kusimamia uingizwaji wa sukari kutoka nje. Haiwezekani sukari inayozalishwa ndani ikakosa soko kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka nje. Hatuwezi kumfurahisha mtu mmoja huku wengi wakiumia,” amesema Majaliwa.

“Viwanda vinasaidia katika kuondoa tatizo la ajira, vinawapa wakulima soko la uhakika la mazao yao pamoja na serikali kupata kodi ya uhakika,” ameongeza kiongozi huyo huku akitaka viwanda vya ndani vilindwe kwani serikali imejikita katika kukuza uchumi wa viwanda.

Amesema kitendo cha wizara hiyo kushindwa kuratibu vizuri suala la uingizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi kutakwamisha uwekezaji jambo ambalo ni sawa na kuihujumu serikali kwa kuwa itasababisha wananchi kupoteza ajira pamoja na serikali kukosa mapato.