Wanafunzi Elimu ya Juu kukaa maghorofa ya NSSF Kijich

0
206

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amekabidhiwa rasmi maghorofa 32 ya NSSF yatakayotumika kwa ajili ya kutoa huduma ya Hosteli kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana, Kazi na Watu wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema mpango huo wa NSSF umetokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ambapo Wizara yake ilisimamia utekelezaji wake huku akieleza kuwa awamu ya pili NSSF watakamilisha majengo ambayo yatawezesha wanafunzi wengine zaidi ya 4000 kuishi.

Nae Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amemshukuru na kumpongeza Rais kwa uamuzi huo na kuongeza kuwa hiyo ni moja tu ya hatua kubwa anazoendelea kuchukua katika kuboresha Sekta ya Elimu. Profesa Ndalichako amesema hatua hiyo itapunguza changamoto ya uhaba wa Hosteli za wanafunzi wa Elimu ya juu hapa Dar es Salaam na ameishukuru na kupongeza Bodi na Uongozi wa NSSF kwa utekelezaji wa haraka wa agizo hilo na kukamilisha mahitaji muhimu ya miundombinu katika majengo hayo kwa wakati.

Majengo hayo yako eneo la Mtoni Kijichi, Wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam na yatahudumia wanachuo 4,317 kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo cha Usimamizi wa fedha IFM, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA)Chuo cha Diplomasia na Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam.