Rais John Magufuli leo Oktoba Pili ametekeleza ahadi yake ya kutoa shilingi milioni Ishirini kwa ajili ujenzi wa ofisi ya wavuvi wadogo (UWAWAKI) waliopo katika eneo la Feri wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam.
Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo Oktoba Mosi hapo jana alipokutana na wajasiriamali hao wakati akifanya mazoezi ya jioni pamoja na mke wake Mama Janeth Magufuli ambaye pia ametekeleza ahadi yake ya kutoa shilingi milioni Tano kwa akina mama wajasiriamali wanaofanya biashara ndogo hasa ya Mamalishe katika eneo hilo.
Fedha hizo zimekabidhiwa na Katibu wa Rais Ngusa Samike kwa Makamu Mwenyekiti wa UWAWAKI, – Amir Amani na kiongozi wa akina Mama wajasiariamali Ashura Nanjonga na kushuhudiwa na mkuu wa wilaya ya Ilala, – Sofia Mjema na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, – Tulusubisya Kamalama.
Kabla ya kukabidhi fedha hizo, Ngusa amesema kuwa pamoja na kutoa fedha hizo Rais Magufuli ameiagiza manispaa ya Ilala impelekee taarifa ya mapato na matumizi ya soko la samaki la Feri haraka iwezekanavyo na amemuagiza Mkuu wa wilaya na Manispaa ya Ilala kushughulikia kero za wavuvi na wajasiriamali wa eneo hilo ikiwemo ushuru wenye kero na tatizo la vyoo.
Makamu Mwenyekiti wa UWAWAKI, -Amir Amani na kiongozi wa akina mama wajasiriamali wa Feri, – Ashura Nanjonga wamemshukuru Rais Magufuli kwa kuwasaidia fedha hizo na kwa kuwajali wao pamoja na Watanzania wengine hasa wanyonge.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, -Sofia Mjema amemshukuru Rais Magufuli kwa kutembelea soko la Feri na kuwasaidia wajasiriamali wa soko hilo na amesema kuwa yeye na timu yake ya viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ilala wataanza mara moja kushughulikia kero za wajasiriamali hao.