Waziri Mkuu wa Lesotho kujiuzulu

0
452
Thomas Thabane alishinda uchaguzi mwaka 2017 baada ya Pakalitha Mosisili kushindwa katika kura ya kutokuwa na imani. [Picha: Getty]

Waziri Mkuu wa Lesotho, Thomas Thabane ametangaza kwenye chama chake (All Basotho Convention-ABC) kwamba atajiuzulu.

Msemaji wa ABC ambacho ndicho chama tawala amesema kuwa Thabane atatangaza rasmi kujiuzulu Jumanne katika baraza ka mawaziri.

Hakuna sababu yoyote iliyotolewa kwa kiongozi huyo kujiuzulu, lakini juma lililopita chama chake kilimtaka ajiuzulu baada ya nyaraka za mahakama kumtuhumu kuhusika katika mauaji ya aliyekuwa mke wake, Lipolelo Thabane.

Kiongozi huyo hajazungumza chochote kuhusu tuhuma hizo, na sasa mke wake mpya, Maesaiah Thabane anatafutwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusu mauaji ya Lipolelo yaliyotokea mwaka 2017.

Inadaiwa kuwa wawili hao, Maesaiah Thabane na Lipolelo Thabane walikuwa wakigombea kuhusu nani ni mke wa kiongozi huyo (first lady). Mahakama ilitoa uamuzi kuwa Lipolelo ndiye mke halali wa kiongozi huyo lakini aliuawa siku mbili kabla ya kuapishwa mumewe.