Mbunge wa Jimbo na Newala Vijijini, Rashidi Ajali Ahkbar amefariki dunia leo Januari 15, 2020 eneo la Mnazi Mmoja mkoani Lindi.
Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Selemani Sankwa amesema chama hicho kinautambua mchango wa kiongozi huyo enzi za uhai wake kwa kuwatumikia wananchi wa Newala Vijijini na kujenga chama hicho.
Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa taarifa za mazishi zitatolewa baada ya makubaliano ya familia na Ofisi ya Bunge.
Chama hicho kimetoa pole sana kwa wafiwa na kinawatakia subira na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu, na Mwenyenzi Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi.