Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango ameiagiza Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kuharakisha mchakato wa kufunga mita za kupima mafuta – Flow Meters katika bandari ya Tanga na kuharakisha urasimishaji wa bandari bubu nne katika mwambao wa bahari wa Tanga ili kudhibiti magendo na upotevu wa mapato ya serikali.
Dkt Mpango ametoa agizo hilo alipotembelea bandari ya Tanga kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa bandari hiyo inayotajwa kuwa moja ya eneo muhimu na chanzo kikubwa cha mapato ya serikali lakini mchango wake hauonekani ipasavyo.
Amesema kuwa mchakato wa kumpata mzabuni wa kufunga mitambo hiyo umechukua muda mrefu licha ya kwamba uongozi wa juu wa serikali ulitoa maelekezo ya kufungwa mara moja kwa flow meter hizo.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, -Donald Ngaile amemweleza Dkt Mpango kuwa mfumo wa kupima mafuta kwa njia ya flow meter haufanyikazi tangu ufungwe miaka mitatu iliyopita kwa sababu ya uchakavu.
Dkt Mpango pia ameuhimiza uongozi wa TPA kuharakisha urasimishaji wa bandari nne bubu zilizoko bahari ya hindi katika mwambao wa Tanga kwenye wilaya za Muheza, Pangani na Mkinga ili kudhibiti biashara ya magendo inayoikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi.