Iran yawakamata waliodungua ndege ya Ukraine

0
381
wananchi Iran waandamana baada ya Iran kukubali kuhusika na ajali ya ndege ya Ukraine. [Picha: Aljazeera]

Iran inawashikilia wanajeshi waliohusika katika kudungua ndege ya Ukraine na watu wengine 30 wanashikiliwa kwa madai ya kuhusika katika maandamano yaliyoanza mara baada ya jeshi kukiri kuhusika na ajali hiyo.

Tukio la kuanguka kwa ndege ya Ukraine iliyopelekea vifo vya watu 176 lilitokea Januari 8, mwaka huu kimakosa na kupelekea mtikisiko nchini humo kutokana na kukosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa, lakini pia wananchi wakiandamana kuilaani serikali yao kwa madai ilitaka kuficha tukio hilo.

Jeshi la Iran liliilenga kwa kombora ndege hiyo kutokana na tahadhari waliyokuwa wakichukua kwani walikuwa wameshambulia kambi mbili za jeshi la Marekani nchini Iraq muda mchache kabla ya tukio hilo.

Waandamanaji ambao wengi wao ni wanafunzi wamekuwa wakiandamana tangu kutokea kwa tukio hilo, miongoni mwa matakwa yao ni kung’oka madarakani kwa kiongozi mkuu, Ayatollah Ali Khamenei ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 30.