Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ukamilishe mapema uchunguzi dhidi ya mapungufu yaliyoibuliwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 na wizi uliofanywa na viongozi wa AMCOS kwa wakulima wa ufuta na korosho ikiwemo wilaya ya Ruangwa.
Ameyasema hayo jana, Jumatatu, Januari 13, wakati akizindua jengo la TAKUKURU, Wilaya ya Ruangwa ambapo ameitaka taasisi hiyo kuwa imara na kuweza kutembea kifua mbele katika mapambano hayo.
Majaliwa ameshuhudia kazi nzuri waliyoifanya TAKUKURU na wanayoendelea kuifanya kupitia uchunguzi na ufuatiliaji wa madai ya malipo ya wakulima wa zao la ufuta na korosho. “Kamilisheni chunguzi hizi zote kwa wakati ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wale wote waliopatikana na hatia.”
Ameongeza kuwa tafiti za hivi karibuni zilizofanywa na wadau wa mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora kama vile Transparency International (TI), MO Ibrahim na Afrobarometer zinaonesha kuwa kwa miaka mitatu mfululizo, yaani 2016 hadi 2018 Tanzania imeendelea kufanya vyema katika mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora.
Pamoja na hayo, waziri mkuu ameagiza kuanzishwa kwa vilabu vya kupambana na rushwa katika shule ili wanafunzi waweze kuwa na uelewa na kuweza kutoa taarifa za rushwa.