China yazitaka Marekani na Umoja wa Ulaya kuiondolea vikwazo Zimbabwe

0
396
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi (kushoto) akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Sibusiso Moyo (kulia) katika mkutano na vyombo vya habari jijini Harare, Zimbabwe, Januari 12, 2020. [Picha: China Plus]

Waziri wa Mambo ya Nje wa China amezitaka Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani (US) kuondoa vikwazo ilivyoweka dhidi ya Zimbabwe kwa sababu havina mantiki katika sheria za kimataifa.

Wang Yi ametoa kauli hiyo wakati akiwa ziarani nchini Zimbabwe

“Vikwazo vilivyowekwa na nchi na taasisi dhidi ya Zimbabwe havina matinki katika sheria ya kimataifa na pia vinakiuka haki za kimaendeleo na maslahi ya Zimbabwe,” alisema Wang Yi kwa mujibu wa Bloomberg.

Waziri huyo aliwasili nchini Zimbabwe Jumamosi, Januari 12, 2020 kama sehemu ya ziara yake katika nchi 5 za Afrika ambapo tayari ameshatembelea Misri, Djibouti na Eritrea, na sasa anatarajia kutembelea Burundi.

Oktoba 2019 mamlaka nchini Zimbabwe zilitangaza siku moja ya mapumziko ambapo ziliwahimiza wananchi kuandamana kupinga vikwazo hivyo.

Marekani na Umoja wa Ulaya zimeendelea kuvishikilia vikwazo hivyo kwa madai ya kuzorota maendeleo ya kidemokrasia, ukiukwaji wa haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari nchini humo. Vikwazo hivyo vinawalenga watu binafsi pamoja na mashirika.

Vikwazo vya kiuchumi na kusafiri vya Marekani kwa sasa vinawahusu watu 85 ikiwa ni pamoja na Rais Emmerson Mnangagwa. Pia kuna kampuni au taasisi 56 ambazo zimewekewa vikwazo.