Idadi ya waliokufa Indonesia yaongezeka

0
2100

Zaidi ya watu 840 wamethibitika kufa baada ya tetemeko la ardhi na tetemeko chini ya bahari – Tsunami kupiga katika maeneo kadhaa nchini Indonesia.

Habari kutoka nchini Indonesia zinasema kuwa juhudi za kuwatafuta watu walionusurika katika tetemeko hilo zinaendelea huku idadi ya watu waliokufa ikitarajiwa kuongezeka.

Idadi ya watu waliokufa katika tetemeko hilo nchini Indonesia inatarajiwa kuongezeka kwa kuwa mpaka sasa maeneo mengi hasa ya vijijini  yaliyokumbwa na tetemeko hilo hayajafikiwa na vikosi vya uokoaji.

Katika mji wa Palu, vikosi vya uokoaji vinajaribu kuwafikia mamia ya watu ambao wanadhaniwa kuwa wako hai huku wakiwa wamefukiwa kwenye vifusi vya miundombinu mbalimbali.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mji huo wa Palu,  Rais Joko Widodo wa Indonesia amewaagiza viongozi wa mji huo kushirikiana na serikali kuu kutoa mahitaji yote muhimu kwa wakazi wa mji huo pamoja na kufanya matengenezo ya miundombinu iliyoharibiwa.

Kwa mujibu wa Shirika la msalaba mwekundu, takribani watu milioni moja nukta sita wameathiriwa na tetemeko hilo la ardhi pamoja na tetemeko la chini ya bahari –  Tsunami na kwamba madhara ya tetemeko hilo yanaweza kuwa makubwa zaidi.