Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekabidhi hati mia moja za Kimila kwa wakulima wadogo wa kijiji cha Litoa kilichopo katika jimbo la Peramiho wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma na kuwataka wamiliki wake kuzitunza na kuzitumia hati hizo kujiletea maendeleo.
Akizungumza wakati wa kuwakabidhi hati hizo katika kijiji cha Litoa wilaya ya Songea vijijini akiwa kwenye shughuli za kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi ya ujenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa katika mikoa ya kusini jana, Naibu Waziri Mabula amewataka wakulima waliokabidhiwa hati hizo kutouza ardhi zao kwa nia ya kupata fedha za haraka.
Aidha, Naibu Waziri Mabula amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji ili kuwa na matumizi bora ya ardhi.