Nyamilandu mjumbe mpya Baraza Kuu FIFA

0
2037

Rais wa chama cha soka cha nchini Malawi,- Walter Nyamilandu amechaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) atakayeliwakilisha Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).

Katika uchaguzi huo uliofanyika nchini Misri, Nyamilandu amepata kura 35 na kumshinda Danny Jordaan ambaye ni Rais wa chama cha soka nchini Afrika Kusini aliyepata kura 18 baada ya mizunguko miwili ya upigaji kura kukamilika.

Katika uchaguzi huo kulikuwa na mizunguko mitatu ya upigaji kura ambapo katika mzunguko wa kwanza walikuwepo wagombea watatu akiwemo aliyekuwa rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), – Leodgar Tenga ambaye aliondolewa katika raundi ya kwanza.

Rais wa shirikisho la soka nchini Kenya, -Nick Mwendwa na yule wa chama cha soka nchini Seychelles,- Elvis Chetty walijitoa katika kinyang’anyiro hicho mapema kabla ya upigaji kura katika mzunguko wa kwanza.

Baraza Kuu la FIFA ndilo lenye dhamana ya kuendesha na kusimamia shughuli zote za mpira wa miguu duniani na wajumbe wake hutoka katika mashirikisho ya soka kwenye mabara yote.

Uchaguzi huo umefanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa rais wa chama cha soka nchini Ghana, -Kwesi Nyantakyi aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya kupokea rushwa ya dola elfu 65 za kimarekani kutoka kwa mwandishi wa habari aliyejifanya ni mwekezaji wa soka.