Ligi kuu Bara kuendelea leo

0
2011

Ligi kuu Tanzania Bara inaendelea kutimua vumbi leo Jumatatu kwa michezo Sita kuchezwa katika viwanja tofauti.

Vinara wa ligi hiyo Mbao FC wenye alama 14 wanasafiri hadi kwenye dimba la Mabatini pale Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani kumenyana na wenyeji Ruvu Shooting wenye alama tano huku maafande wa JKT Tanzania wakiwa nyumbani kwenye dimba la Jenerali Isamuhyo kuwaalika African Lyon.

Michezo mingine,  chama la wana Stand United watakuwa nyumbani kwenye dimba la Kambarage mjini Shinyanga kukipiga na Mbeya City wakati wakulima wa alizeti Singida United wakiwa kwenye dimba la Namfua mjini Singida kuwaalika wanapaluhengo Lipuli FC ya Iringa.

Wagosi wa kaya Coastal Union wenyewe wana kibarua cha kukabiliana na Mwadui FC,  mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga wakati wana tamtam Mtibwa Sugar wakiwa katikati ya mashamba ya miwa huko Turiani wilayani Mvomero mkoani Morogoro wakiwakaribisha Biashara United ya Mara kwenye dimba la Manungu Complex.

Katika mchezo pekee wa ligi hiyo uliochezwa jana kwenye dimba la Taifa jijini Dar es salaam, watani wa jadi Simba na Yanga wameshindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu katika mchezo ambao kwa kiasi kikubwa ulitawaliwa na Simba walioshindwa kuzitumia nafasi walizopata kufunga huku mlinda mlango wa Yanga, Beno Kakolanya akiibuka shujaa wa mchezo huo.