Vyombo vya Dola vinamshikilia mmiliki wa VICOBA Foundation kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma za wizi zinazomkabili.
BoT imesema kumekuwa na kampuni za kitapeli zinazodai kutoa mikopo kwa wananchi ndani ya muda mfupi baada ya kujiunga kwa kuweka amana kwa njia ya mtandao.
Taarifa ya BoT imebainisha kuwa kampuni hizo ni pamoja na ile inayojiita VICOBA Foundation inayojinasibu kutoa mikopo ya kuanzia TZS 2,000,000 hadi TZS 10,000,000 baada ya mteja kulipia ada ya kujiunga ya kati ya TZS 200,000.00 hadi 500,000.00.
Uchunguzi wa awali wa BoT unaonesha kwamba kampuni hiyo imekuwa ikiudanganya umma kwamba ni taasisi ya serikali ili kuvuta wateja, lakini haina hata ofisi ya kudumu, na pia imekuwa ikitumia majina ya viongozi waandamizi wa serikali yakiwemo majina ya Rais Dkt Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kufanikisha utapeli wao.