MBUNGE wa Jimbo la Busega lililopo Mkoani Simiyu, Dkt. Rafael Chegeni amewataka Vijana kuchangamkia fursa za kiuchumi zitokanazo na Utalii kupitia tamasha la kukuza na kuendeleza Utalii Wilaya ya Busega la ‘Lamadi Utalii Festival’ lililokuwa likifanyika kwa siku nne katika shule ya Msingi Itongo, mjini Lamadi.
Akizungumza wakati alipokuwa mgeni rasmi katika kilele cha tamasha hilo, Dkt. Rafael Chegeni alieleza kuwa, vijana wengi wapo tu mitaani bila kujishughulisha wakiwemo wengine kucheza ‘pooltable’ hivyo ni wakati sasa kuanza kubuni vitu mbalimbali vitokanavyo na fursa katika Utalii.
“Huu ni mwanzo tu Tamasha la Lamadi Utalii liwe chachu kwenu. Mji utakuwa kwa kasi zaidi kama miji mingine ya kitalii kama ilivyo Karatu hivyo mchangamkie fursa na nyie hapa Lamadi.
Muanze kubuni na kutengeneza vitu mbalimbali ili hata watalii wanaoweza kuja hapa waweze kuviona na kuvutiwa waweze kununua, wakiweza kununua namna hii mtapata kipato kwa hiyo wito wangu kwa vijana wote sasa sio muda wa kulala ni muda wa kuchapa kazi” alisema Dkt. Chegeni.
Aidha, katika hatua nyingine, Dkt. Chegeni kupitia ofisi yake ya Mbunge, ameahidi kutoa kiasi cha Tsh. Laki Tano kwa ajili ya kusaidia mafunzo kwa vijana wote watakaopenda kujifunza mambo ya kuongoza watalii ‘Tour guide’ kwa muda mfupi.
