Kiongozi wa Korea kaskazini, Kim Jong Un, ametaka kuwepo kwa hatua za haraka na za kujilinda, kuelekea muda wa mwisho uliowekwa wa kumalizika kwa mazungumzo na Marekani kuhusu kuachana na mpango wake wa Nyuklia.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la Korea Kaskazini,- (KCNA), Kim ameitisha mkutano wa maofisa wa ngazi za juu wa chama tawala kujadili masuala ya kisera, huku wasiwasi ukiongezeka juu ya muda wa mwisho wa kuitaka Marekani ilegeze msimamo wake kwenye mazungumzo hayo.
Kim amependekeza hatua kadhaa za kuchukuliwa kwenye maeneo ya sera za nje, silaha na jeshi.
Korea Kaskazini inaitaka Marekani kuchukuwa mwelekeo mpya kwenye meza ya mazungumzo huku ikionya kwamba itachukua hatua mpya endapo serikali ya Trump itashindwa kutimiza matwaka yao.