Mbunge wa Busega, Dkt. Rafael Chegeni anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha tamasha kubwa la kukuza na kuendeleza Utalii la ‘LAMADI UTALII FESTIVAL.’
Mwenyekiti wa Kamati wa Tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Busega Tano Mwera ametoa taarifa hiyo kwrnye mahojiano na kituo kimoja cha Radio, kuwa wanamtarajia kuwa na Mbunge wa jimbo hilo katika viwanja vya shule ya Itongo siku ya Januari Mosi, 2020.
“Siku ya kilele Januari Mosi tutajumuika pamoja na mgeni rasmi ambaye atalifunga tamasha letu, Mbunge Dkt. Rafael Chegeni katika viwanja vya Shule ya Itongo.” Ameeleza Mkuu wa Wilaya, Tano Mwera.
Katika siku hiyo ya kilele pia kutakuwa na shughuli za safari za kitalii ikiwemo ya kwenda Hifadhi ya Serengiti kwa malipo ya gharama nafuu.
“Siku ya kilele Januari Mosi, 2020 tutakuwa na tukio la kwenda hifadhi ya Serengeti na gharama ni shilingi 55,000, kwa kila Mtanzania lakini watoto 10 wa mwanzo wao watalipiwa shilingi 50,000 pekee kama ofa.
Awali kabla ya kilele, tamasha hilo, Desemba 3, kutakuwa na shughuli mbalimbali zikiwemo Utalii wa kuzunguka ziwa Victoria na boti ‘Boat Cruising’ ambapo gharama itakuwa Tsh. 10,000 kwa Mtanzania na muda ni masaa matatu kwenye maji.
Pia kutakuwa na Biking kwa gharama ya Tsh. 5000 kwa kila Mtanzania ikijumuisha kukodi baiskel kwa nusu siku pamoja na maji ya kunywa ambapo itaanza saa 12 asubuhi hadi mida ya saa 5 asubuhi.