Rais Magufuli Atuma Salamu za Krismas akiwa Chato

0
385

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 22 Desemba, 2019 ameungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Chato Mkoani Geita kusali Dominika ya 4 ya Majilio na ametumia nafasi hiyo kuwatakia heri ya Krismasi na Mwaka Mpya Watanzania wote.

Katika salamu hizo, Rais Magufuli amesema tunapoelekea katika sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya Wakristo na Waumini wa madhehebu mengine mbalimbali wanalo jukumu la kuendelea kuombea amani, upendo na umoja kwa wanadamu wote bila kubaguana.

“Niwaombe ndugu zangu wa Chato na Watanzania kwa ujumla, tusherehekee sikukuu ya Krismasi kwa amani na upendo mkubwa, lakini pia tuukaribishe Mwaka Mpya kwa amani na upendo mkubwa wa Kristo, mwaka unaokuja uwe mwaka wa mafanikio, uwe mwaka wa maendeleo, uwe mwaka wakujenga umoja wetu kwa Watanzania wote, uwe mwaka wa amani na upendo na uwe mwaka wa kuendeleza Taifa letu katika maendeleo ya kweli”amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli
amewapongeza Waumini wa Parokia ya Bikira Maria Chato kwa kazi kubwa ya upanuzi wa Kanisa wanayoendelea nayo ambayo naye alichangia upanuzi wake mwaka 2016.

Misa Takatifu hiyo imeongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Henry Mulinganisa.