Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga amesema kuwa, utaratibu mpya wa vifurushi vya bima ya afya hauondoi taratibu zilizowekwa na Serikali katika kugharamia matibabu kwa watu wasiojiweza wakiwemo Wazee.
Konga ametoa kauli hiyo mkoani Mtwara wakati wa mkutano na Wanachama wa Chama cha Waandishi wa habari wa mikoa ya Lindi na Mtwara, baada ya Waandishi hao wa habari kutaka kufahamu ni kwanini gharama za matibabu kwa Wazee kwenye vifurushi vipya vya Bima ya Afya ni tofauti na makundi mengine.
“Hata Sera ya Afya ya mwaka 2007 ukurasa wa 29 unasema Serikali inatambua uwepo wa watu wasio na uwezo kutoka makundi ya Watoto, Wazee na kina Mama Wajawazito, na utaratibu huu unalenga Wazee wenye uwezo na hauondoi taratibu za Serikali za kugharamia makundi hayo, ndio maana utaratibu wa msamaha kwa makundi hayo bado upo na unaendelea kama kawaida” amesema Konga.

Ameongeza kuwa, gharama za matibabu kwa Wazee kwenye vifurushi vipya vya Bima ya Afya ni tofauti na makundi mengine kutokana na hali halisi kuwa kadiri umri unavyokwenda ndivyo mahudhurio ya hospitalini yanaongezeka na uhalisi wa gharama za matibabu zinakuwa kubwa zaidi.
“Utaratibu huu hauangalii uwezo wa kulipia fedha bali unaangalia uhalisia wa gharama za matitabu, matatizo ya figo, matatizo na moyo mara nyingi yanakuwa kwa watu wenye umri kuanzia miaka hamsini na kuendelea, leo hii ugonjwa mfano wa tezi dume, gharama zake ni kubwa sana” ameongeza Mkurugenzi Mkuu huyo wa NHIF.
Awali akiwasilisha mada kwa Waandishi wa Habari, Meneja Masoko na Huduma kwa Wateja kutoka NHIF Hipoliti Lello amesema kuwa, Serikali imedhamiria kuhakikisha kila Mtanzania anajiunga na Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya na ndio maana umeweka utaratibu wa vifurushi vyenye gharama ya kuanzia Shilingi Laki Moja na Tisini na Mbili Elfu.
“Mwanzo tulikuwa na utatibu wa kulipa Shilingi Milioni Moja na Nusu kujiunga kwa mtu mmoja, lakini ilikuwa ni changamoto kubwa kwa mtu mmoja mmoja na ndio maana tumeishusha hadi kufikia Shilingi Laki Moja na Tisini na Mbili Elfu, hii yote ni dhamira ya dhati ya kuhakikisha tunamrahisishia Mtanzania kujiunga na Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya” amesema Lello.
