Maandamano mapya yamezuka katika mji wa New Delhi na miji mingine nchini India, huku Waandamanaji wakiwa na hasira baada ya Mahakama Kuu nchini humo kuahirisha shauri la Wahamiaji lililofikishwa mahakamani hapo.
Mahakama Kuu nchini India imesema kuwa, inapaswa kupata maelezo ya kina kutoka Serikalini kabla ya kusikiliza shauri linalohusu Muswada uliopitishwa na Mabunge yote mawili ya nchi hiyo unaotoa ridhaa ya ukimbizi wa kisiasa kwa watu wanaokabiliwa na mateso katika nchi zao.
Hata hivyo muswada huo unaosubiri kuwa sheria, hautoi ridhaa ya kuwapatia hifadhi ya kisiasa Wakimbizi wanaopata mateso ya kidini nchini mwao, ambao ni Waumini wa dini ya Kiislamu.
Hatua hiyo imezusha hasira miongoni mwa Wananchi wa India wanaoona kuwa Muswada huo ni wa kibaguzi.
India imedhamiria kuwapatia hifadhi ya kisiasa Wakimbizi kutoka nchi za Pakistan, Afghanistan na Bangladesh wanaopata mateso kutokana na imani zao, wengi wao wakiwa ni kutoka katika madhehebu ya Hindu na Budha.
