RC. Chalamila: Afya Sio Siasa, Jiungeni Na Vifurushi Vya Bima Ya Afya

0
200

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila amewataka watanzania kujikatia Bima ya Afya kwa mpango wa vifurushi kuwapuuza baadhi ya watu wanaohusisha siasa na mpango huu ulioletwa kuwafikia watanzania wengi zaidi.

Chalamila ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya katika uwanja wa stendi ya Kabwe, Jijini Mbeya.

Awali akiongea katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Anne Makinda amesema kuwa tangu kuzinduliwa kwa mfuko huu muitikio wa watanzania umekuwa ni mkubwa na Mfuko upo katika utaratibu wa kuanzisha mpango wa DUNDULIZA ambao utawawezesha watanzania kujiwekeaa fedha kidogkidogo  hadi akamilishe kulipia bima yake.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Christopher Mapunda amesema kuwa uanzishwaji wa Vifurushi ni fursa kwa wananchi kujiunga na bima ya afya kuanzia kiwango cha 192,000 na kuwawezesha kupata huduma ya uhakika ya matibabu hasa kutokana na kuongezeka kwa gharama za matibabu siku hadi siku.

Akiongea baada ya kupatiwa kadi ya Bima ya Afya Emanuel Mushi amesema kuwa mpango huu ni mzuri kwani afya ni muhimu na mpango huu wa vifurushi ni mzuri kutokana na kupungua kwa gharama kutoka Milioni moja na laki Tano hadi sasa imepungua na kufikia Shilingi laki moja na tisini na mbili kwa mtu mmoja.