Michango zaidi yaendelea kutolewa

0
2411

Michango zaidi inaendelea kutolewa na taasisi pamoja na watu mbalimbali kufuatia kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere Septemba 20 mwaka huu katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Akizungumza na TBC kutoka kisiwani Ukara, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi  na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa mpaka sasa akaunti ya maafa imepokea jumla ya shilingi milioni 557.

Amesema miongoni mwa michango iliyopokelewa hii leo, ni pamoja na shilingi milioni 125 kutoka benki ya KCB na shilingi milioni kumi kutoka Benki ya Posta.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kamwelwe, kwa siku ya leo pekee akaunti hiyo ya maafa  imepokea jumla ya shilingi milioni 160.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesisitiza kuwa fedha hizo zitatumika kama ilivyokusudiwa.

Kuhusu kazi ya kunasua kivuko hicho cha MV Nyerere, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa kazi hiyo iko katika hatua ya mwisho ambayo ni kukinyanyua na kwamba kitanyanyuliwa muda mfupi ujao.