Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa anatarajia kukutana kwa mara ya pili na Rais Kim Jong-un wa Korea Kaskazini katika siku za hivi karibuni.
Akizungumza na Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini mjini New York nchini Marekani, Trump amesema kuwa mambo mazuri yamekwishafikiwa toka akutane kwa mara ya kwanza na kiongozi huyo wa Korea Kaskazini nchini Singapore.
Kwa mujibu wa Trump, uhusiano kati ya Marekani na Korea Kaskazini umezidi kuimarika hasa baada ya mkutano wake na Rais Kim mwezi June mwaka huu, mkutano ambao ameuita kuwa ulikua ni wa kihistoria.
Amesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ataandaa mkutano mwingine kati yake na kiongozi huyo wa Korea Kaskazini hivi karibuni bila kueleza utafanyika wapi.