Ndege iliyokua ikishikiliwa Canada yaachiliwa

0
223

Ndege ya Tanzania aina ya Bombardier Q 400 iliyokuwa ikishikiliwa nchini Canada tangu mwezi Novemba  mwaka huu, imeachiliwa na itawasili nchini wakati wowote na kupokelewa mkoani Mwanza.

Kauli hiyo imetolewa mkoani Mwanza na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Rais John Magufuli,  wakati wa ufunguzi wa majadiliano ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM  Taifa na kuongeza kuwa tarehe ya kupokelewa kwa ndege hiyo itatangazwa hapo baadaye.

Novemba 23 mwaka huu  huko mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali Duniani,  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi alitangaza kukamatwa kwa ndege hiyo na kusema kuwa kesi iko mahakamani nchini Canada.

Profesa Kabudi alisema kuwa, aliyesababisha ndege hiyo kukamatwa nchini Canada ni Mkulima Hermanus Steyn,  ambaye alifungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini akidai fidia ya Dola Milioni 33 za Kimarekani kutoka nchini Tanzania.

Kesi hiyo ilisababisha Mahakama hiyo ya Afrika Kusini  kutoa amri ya kuzuiliwa kwa ndege ya Tanzania aina ya Airbus A220 –  300 katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo uliopo nchini humo mwezi Agosti mwaka huu.