Mabadiliko ya Tabianchi yaendelea kuiathiri Tanzania

0
196

Tanzania imetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua za haraka na za pamoja kushughulikia suala la mabadiliko ya Tabianchi na athari zake.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mussa Sima,  wakati wa mkutano wa 25 wa Mawaziri wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya Tabianchi unaondelea huko Madrid nchini Hispania.

Amewataka Wajumbe wanaoshiriki katika mkutano huo kuendelea kuchukua hatua zaidi ili kushughulikia changamoto za mabadiliko ya Tabianchi.

 “Tunahitaji kuendeleza kasi ya kushughulikia mabadiliko ya Tabianchi kwa kubainisha malengo mahususi ya kupunguza tatizo hilo kwa kuchukua hatua zote muhimu zinazohitajika” amesisitiza Naibu Waziri Sima.

Aidha ameeleza kuwa athari za mabadiliko ya Tabianchi tayari zimeanza kuonekana Tanzania kupitia matukio makubwa ya hali ya hewa ikiwemo kunyesha kwa mvua kubwa na kuongezeka  kwa joto, mambo ambayo yanasababisha mafuriko na kusambaa kwa magonjwa ambukizi, upotevu wa mali na maisha ya wanadamu na uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo mengi.

Naibu Waziri Sima amebainisha kuwa kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), mwezi Oktoba mwaka huu umekuwa na mvua nyingi ulikinganisha na kipindi kingine kama hicho kwa karibu muongo mmoja uliopita na kuathiri sekta zote muhimu kama vile Kilimo, Afya, Uvuvi, Mifugo, Maji na Afya na hivyo kuongeza magonjwa ikiwa ni pamoja na dengue na malaria.