Shindano la makala kwa waandishi wa Habari

0
236

Shirika la Posta Tanzania limeandaa shindano la uandishi wa makala kwa waandishi wa habari lengo likiwa ni kuelezea umuhimu wa anuani za makazi katika kujenga Tanzania ya viwanda.

Kaimu Posta Masta Mkuu wa shirika hilo, Mwanaisha Said amesema hayo hii leo Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka 40 ya PAPU.

Amesema shindano hilo limeanza rasmi jana na litamalizika Disemba 31 mwaka huu.

Amesema washindi 10 watachaguliwa katika shindano hilo ambao makala zao ni bora zaidi na watapata zawadi mbalimbali zikiwemo kompyuta mpakato, simu tanashati, kamera, vyeti na fedha taslimu.

“Washindi watatu wa awali watakabidhiwa zawadi zao na mgeni rasmi ambaye ni Rais John Magufuli siku ya kilele cha maadhimisho ya sherehe hiyo itakayofanyika Arusha Januari 18, mwakani,” amesema.

Ameongeza kuwa Makala bora kabisa ya mshindi wa kwanza itasomwa mbele ya rais Magufuli siku hiyo ya kilele, pia makala zote tatu zitachapishwa kwenye moja ya magazeti yanayochapishwa kila siku hapa nchini.

“Nitoe wito kwa wenzetu waandishi wa habari hususan waandishi wa Makala, basi mchukue fursa hiyo kuonyesha umahiri wenu mbele ya Rais wetu na mbele ya wawakilishi mbalimbali kutoka nchi wanachama wa umoja huo barani Afrika watakaohudhuria maonyesho hayo,” amesisitiza.

Naye Meneja Mkuu Rasiliamali za Shirika hilo, Marcus Mbogo amesema katika maadhimisho hayo Posta itatambua mchango wa Baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuanzisha umoja huo.