Waziri wa Kilimo, – Japhet Hasunga ametangaza kuifuta Bodi ya Wakala wa Mbegu za Kilimo Nchini (ASA) endapo itashindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuzalisha Tani Elfu Tano za mbegu za kilimo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020.
Waziri Hasunga ametoa kauli hiyo mkoani Morogoro wakati akizungumza na Watumishi wa Wakala huo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani humo.
Amesema kuwa pamoja na ASA kuongeza eneo la uzalishaji wa mbegu kutoka hekta 9, 890 mpaka kufikia hekta 10,115.2, bado uzalishaji ni mdogo kwa kuwa Wakala huo unazalisha Tani 1, 440 pekee.
Waziri Hasunga amesisitiza kuwa, zana zote zilizonunuliwa na ASA zinapaswa kutumika ipasavyo, ili kuongeza uzalishaji wa mbegu bora na za kutosha zinazokidhi mahitaji.
“Sisi kama nchi tunahitaji Tani 100,086 za mbegu, na mpaka sasa hivi uwezo wetu wa kuzalisha ndani na kuagiza nje hauzidi Tani 57,000, sasa mahitaji ni makubwa watu wanataka mbegu bora lakini uzalishaji bado upo chini” amesema Waziri Hasunga.
Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Kilimo mbegu bora ndio msingi na mhimili wa kilimo, hivyo ili kubadili kilimo kutoka cha kujikimu na kuwa kilimo chenye tija na cha kibiashara ni lazima kuwa na uzalishaji mkubwa ndani ya nchi.