Watu Wanane wamethibitika kufa nchini Uganda, baada ya kutokea kwa maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Habari zaidi kutoka nchini Uganda zinaeleza kuwa, baadhi ya miili ya watu waliokufa imepatikana kwenye vifusi vya majengo yaliyobomoka pamoja na matope, huku watu wengine zaidi ya Arobaini wakiwa hawajulikani walipo kufuatia maporomoko hayo ya udongo.
Jitihada za kutafuta miili ya watu waliokufa na wale ambao hawajulikani walipo zimekua zikikwamishwa na kutokuwepo kwa miundombinu ya uhakika katika maeneo mengi ya nchi hiyo, ambapo barabara pamoja na madaraja mengi yameharibiwa na mvua hizo zinazoendelea kunyesha.
Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Uganda, zimesababisha takribani watu Elfu Thelathini katika maeneo mbalimbali nchini humo kuyahama makazi yao.