Msichana adhalilishwa na kuunguzwa moto India

0
556

Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 23 katika jimbo la Uttar Pradesh nchini India ambaye ni muathirika wa vitendo vya udhalilishaji, amepata majeraha makubwa ya moto baada ya kuunguzwa na watu wasiojulikana.

Msichana huyo ambaye kwa sasa amelazwa hospitalini akiwa na hali mbaya, ameunguzwa moto akiwa njiani kwenda mahakamani kusikiliza kesi aliyoifungua mwezi Machi mwaka huu dhidi ya Wanaume wawili waliomdhalilisha.

Kufuatia tukio hilo Wanaume Watano akiwemo mtuhumiwa mmoja wa tukio hilo la udhalilishaji, wanashikiliwa na Polisi nchini India kwa tuhuma za kumuunguza moto msichana huyo.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema kuwa, msichana huyo alikua akielekea kituoni kwa lengo la kupanda treni kwenda mahakamani, ndipo walipotokea Wanaume hao Watano ambao walimvuta na kumpeleka katika eneo la jirani lililo na shamba, na kisha kumuunguza moto kabla ya kuokolewa na Wasamaria wema.

Vitendo vya Wanawake kudhalilishwa na kuuawa vimekua vikitokea mara kwa mara nchini India, ambapo mwezi Julai mwaka huu Mwanamke mwingine aliyekua akimtuhumu Mbunge wa jimbo moja nchini humo kwa kumdhalilisha, alijeruhiwa vibaya katika ajali ya barabarani.

Katika tukio hilo ndugu wawili wa Mwanamke huyo walifariki dunia, huku Mwanasheria wake akijeruhiwa, ambapo mpaka sasa polisi nchini India wanaendelea na uchunguzi.

Mwezi Novemba mwaka huu, Msichana mwingine mwenye umri wa miaka 27 mkazi wa mji wa Hyderabad alidhalilishwa na kuchomwa moto, hali iliyozusha maandamano katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, ambapo Waandamanaji hao  walitaka kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya watu wanaofanya vitendo hivyo vya udhalilishaji kwa Wanawake.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Serikali ya India, kwa mwaka 2017 pekee matukio 33,658 ya udhalilishaji dhidi ya Wanawake yaliripotiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, huku wastani ukiwa ni matukio 92 kila siku.