Sarri asema mahusiano yake na Ronaldo ni mazuri

0
1039

Kocha wa Juventus, -Maurizio Sarri amesema kuwa, mahusiano yake na mshambuliaji Cristiano Ronaldo ni mazuri hasa wakati huu ambao kibibi kizee hicho cha mjini Turin kinajiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Atletico Madrid.

Sarri ambaye alimfanyia mabadiliko Ronaldo katika mechi Mbili mfululizo bado hana uhakika kama Ronaldo atakuwa timamu kwa ajili ya mchezo wao wa leo dhidi ya Atletico.

Juventus tayari wamefuzu hatua ya mtoano ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya walipoinyuka Lokomotiv Moscow katika mchezo ambao Ronaldo alifanyiwa mabadiliko na kisha kwenye mchezo uliofuata wa ligi dhidi ya AC Milan alifanyiwa tena mabadiliko kabla ya kwenda kuifungia Ureno mabao Manne katika  michezo  miwili ya kuwania kufuzu Fainali za Euro.

Hata hivyo mshambuliaji huyo hakujumuishwa kwenye mchezo wa Ligi dhidi ya Atlanta mwishoni mwa juma lililopita kutokana na kusumbuliwa na goti na Sarri anasema ingawa amefanya mazoezi na wenzake lakini bado hana uhakika kama ataweza kucheza katika mchezo wa leo.