Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt Admassu Tadesse ameahidi kuwa Benki hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuipatia mikopo yenye masharti nafuu, kwa ajili ya kutekeleza miradi yake ya kimkakati ya maendeleo kwa sababu uchumi wake uko imara na inakopesheka
Dkt Tadesse ametoa ahadi hiyo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango, ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo hususan ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na ujenzi wa mradi wa kufua umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ya mto Ruhudji mkoani Njombe.
Amesema kuwa miezi michache iliyopita TDB iliipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa Dola Bilioni Moja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele inayotekelezwa na Serikali na kwamba wako mbioni kutoa kiasi kingine kikubwa cha fedha hivi karibuni.
Kwa upande wake Dkt Mpango amesema kuwa, Benki hiyo ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika imekuwa mdau muhimu katika maendeleo ya Taifa na kwamba pamoja na Dola Bilioni Moja kupokelewa na Serikali mwezi Agosti mwaka huu, Serikali inatarajia kupata kiasi kingine cha Dola Milioni 300.
Amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kitaelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa (SGR) pamoja na miradi ya kuzalisha nishati ya umeme ili nchi iweze kuimarisha sekta ya uzalishaji viwandani kwa kuwa na umeme wa uhakika.
Tanzania ni mongoni mwa Wanahisa 31 wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini Mwa Afrika, ambapo hadi kufikia Disemba 31 mwaka 2018 Tanzania ilikuwa imeshika nafasi ya Nne ya uwekezaji katika Benki hiyo ikiwa na asilimia 8.33 ya hisa.