Waliopisha ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa kuanza kulipwa fidia Disemba Mosi

0
139

Rais John Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, – Godwin Kunambi kuanzia Disemba Mosi mwaka huu, awe ameanza kuwalipa fidia ya Shilingi Bilioni 3.399  Wakazi 1,500 wa eneo la Kikombo , Chamwino mkoani Dodoma waliotoa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa katika eneo la Kikombo, -Chamwino mkoani Dodoma,

Amesema kuwa wakati fidia zikiandaliwa, Wakazi wanaodai fidia hizo waache kuwasikiliza  watu wasio waaminifu,  ambao wamekua wakiwashawishi kuongeza fidia ya maeneo yao tofauti na tathmini iliyofanyika awali.

Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale,  kutangaza tenda kuanzia wiki ijayo ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 18 kwa kiwango cha lami, ambayo inaenda katika eneo la mradi wa ujenzi huo wa  Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa.