Rais Magufuli awataka Mabalozi 5 aliowaapisha leo kwenda kuchapa kazi

0
192

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewaapisha Mabalozi Watano aliowateua hivi karibu baada ya Mabalozi hao kupangiwa vituo vya kazi.

Mabalozi hao Mhe. Mej. Jen Anselm Shigongo Mlacha aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania Cairo – Misri, Mhe. Mohamed Abdallah Mtonga aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania Abu Dhabi – UAE, Mhe. Dkt. Jilly Elibariki Maleko aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania Bujumbura – Burundi, Mhe. Jestas Abouk Nyamanga aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania Brussels – Ubelgiji na Mhe. Ali Jabir Mwadini aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania Riyadh – Saudi Arabia.

Hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi hao imefanyika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Mhe. Lameck Mlacha na viongozi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge.

Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewatakia heri katika majukumu yao ya kuiwakilisha Tanzania katika nchi walizopangiwa na amewataka kuripoti katika vituo vyao katika kipindi kisichozidi wiki moja.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Mabalozi hao pamoja na Mabalozi wengine wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali kusimamia vizuri fedha na mali zilizopo katika Balozi hizo, na pia kusimamia vizuri utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ili Tanzania inufaike na uhusiano mzuri uliopo kati yake na nchi wanazoziwakilisha.