MOI yaokoa Shilingi Bilioni 38.4 katika kipindi cha miaka Minne

0
208

Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) iliyopo jijini Dar es salaam,  katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya Tano  imeokoa Shilingi Bilioni 38.4 zilizotakiwa kutumika kwa ajili ya kusafirisha zaidi ya Wagonjwa Elfu  43 nje ya nchi kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya upasuaji wa Kibingwa.

Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface na kuongeza kuwa,  katika kipindi hicho Taasisi hiyo imeendelea kuimarisha na kuboresha huduma mbalimbali za afya kwa Wananchi.

“Gharama za matibabu za Wagonjwa hao kwa ndani ya nchi zilikuwa Shilingi Bilioni 16.5 na kama Wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu, jumla ya Shilingi Bilioni 54.9 zingetumika, na hivyo kuifanya Taasisi kuokoa Shilingi Bilioni 38.4 ambazo zitatumika kwa shughuli nyingine za maendeleo”, amesema Dkt Respicious.

Aidha amesema kuwa, katika kipindi hicho cha miaka minne ya  uongozi wa Serikali ya awamu ya Tano,  MOI imeweza kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka Sita  hadi Tisa, kuongeza vyumba 32 vya Wagonjwa binafsi vya daraja la juu,  pamoja na kuongeza chumba cha upasuaji kwa mgonjwa bila kulazimika kulala hospitali.