Mourinho aahidi maajabu Spurs

0
1062

Kocha mpya wa Tottenham Hotspur Mjivuni Jose Mourinho, ameahidi kuleta msisimko na furaha katika Klabu hiyo ya Kaskazini mwa London.

Mreno huyo mwenye umri wa miaka 56 amelamba dili la kuifundisha Spurs jana Jumatano akichukua nafasi ya Mauricio Pochettino, aliyefungashiwa virago usiku wa Jumanne wiki hii.

Kocha huyo wa zamani wa vilabu vya Chelsea na Manchester United amesema kuwa, Wachezaji wa Spurs wana ubora anaotaka na wanakidhi viwango vya daraja la dunia pamoja na kuwa na uwanja mzuri wa mechi na ule wa mazoezi.

Mourinho amesema kuwa kwa sasa ana furaha na anaangalia mbele kukabilina na changamoto mpya, na kwamba hajaenda Spurs kujaribu kwani siku zote yeye si mtu wa majaribio bali anataka kushinda.

Mourinho amesaini mkataba utakaofanya kuhudumu ndani ya Spurs mpaka mwishoni mwa msimu wa 2023, huku akipokea kitita cha Paundi Milioni Nane kwa mwaka.

Hiyo ni kazi ya kwanza kwa Mourinho kama Kocha, tangu alipotimuliwa na Manchester United mwezi Disemba mwaka 2018 na anaichukua Spurs ikiwa katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, na wengi wanasubiri kuona atafanya maajabu gani.