Kipindi changu ni cha Neema kwa Mkulima, asema Rais Magufuli

0
230

Rais John Magufuli amesema kuwa katika kipindi chake cha uongozi kamwe hatompangia Mkulima bei ya kuuza mazao yake.

Akizungumza na Wakazi wa mkoa wa Morogoro akiwa njiani kuelekea jijini Dodoma, Rais Magufuli amesema kuwa, katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha Wakulima wananufaika kwa kupanga wenyewe bei za mazao yao.

Ameongeza kuwa, kama kuna Mfanyabiashara anataka kununua mazao ya Mkulima na kuona bei iko juu, si wakati wa kulalamika bali ni vema akatumia fursa hiyo kujishughulisha na sekta ya Kilimo.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kwa muda mrefu Wakulima nchini wamekuwa wakitaabika na kutumia gharama kubwa katika uzalishaji wa mazao mbalimbali, hivyo katika kipindi chake hataki jambo hilo liendelee.

Ameuagiza uongozi wa mkoa wa Morogoro, mkoa ambao ni miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula kingi, kutumia mvua zinazoendelea kunyesha ili kuzalisha zaidi mazao mbalimbali.