Meya wa jiji la Arusha Kalisti Lazaro ajiunga na CCM

0
150

Wakati kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zikiendelea nchini, Meya wa jiji la Arusha, – Kalisti Lazaro amejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupokelewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, -Humphrey Polepole.

Kalisti aliyefika katika Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es salaam ameeleza kuwa, amefikia uamuzi huo baada ya kupitia wakati mgumu akiwa katika wadhifa wake wa Meya wa jiji la Arusha.

Amedai kuwa, vitisho vya mara kwa mara ikiwamo dhidi ya uhai wake ndio vimepelekea kujivua nafasi zake zote katika Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kujiunga na CCM, chama ambacho kinashughulika na utatuzi wa kero za Wananchi.

Amesema kwa sasa yuko tayari kufanya kazi ya Wananchi akiwa ndani ya Chama ya Mapinduzi.

Kwa kujiunga na CCM, Kalisti amejiuzuru nafasi ya Udiwani, Umeya wa jiji la Arusha, Uenyekiti wa Mameya na Madiwani wote wa Chadema nchini na Ujumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, -Humphrey Polepole imeeleza kuwa, Kalisti atapokelewa rasmi na Wanachama wa CCM mkoa wa Arusha katika tarehe itakayopangwa.