Serikali yahaidi kumsaidia mtoto Anna

0
218

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ametoa pole kwa Anna Zambi mwenye umri wa miaka 16, ambaye amefiwa na Wazazi wake wote Wawili pamoja na wadogo zake Watatu.

Kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa Kijamii wa Twitter, Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo tayari kumpatia Anna msaada wa Kisaikolojia.

“Pole nyingi kwa binti yetu Anna Zambi, hili jambo ni kubwa mno kwa huyu mtoto, inaumiza sana, ninamuombea kwa Mungu ampe nguvu na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu, nasi Wizara ya Afya tukiwa na dhamana ya kusimamia ustawi na maendeleo ya Watoto nchini tunachukua jukumu la kuratibu na kusimamia psychosocial support ya mtoto huyu pamoja na masuala mengine yanayohusu ustawi wake kwa ujumla”, amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Amesema kuwa, leo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt John Jingu na Kamishna wa Ustawi wa Jamii wanaitembelea familia ya Anna inayoishi huko Goba mkoani Dar es salaam na baadaye Serikali itatoa taarifa zaidi kuhusu suala hilo.

Waziri huyo wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amewaombea pumziko la Amani Wazazi na ndugu wote wa Anna ambao wamefariki Dunia katika ajali mbaya ya gari.

Wazazi wa Anna, – Lingston Zambi na Winifrida Lyimo
pamoja na ndugu zake Watatu Lulu, Andrew na Grace walifariki Dunia Oktoba 26 mwaka huu wakiwa njiani kutoka jijini Dar es salaam kuelekea mkoani Kilimanjaro, kwenye Mahafali ya Kidato cha Nne
ya Anna, ambapo gari walilokua wakisafiria lilisombwa na mafuriko huko Handeni mkoani Tanga.