Mkandarasi Simiyu apewa siku 14 kujirekebisha

0
186

Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imempa muda wa siku 14 Mkandarasi wa umeme vijijini mkoani Simiyu, kuongeza kasi ya usambazaji umeme, la sivyo atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kusitishiwa mkataba.

Mwenyekiti wa Bodi ya REA, -Julius Kalolo amesema hayo wilayani Busega mkoani Simiyu mara baada ya kukagua kazi ya usambazaji umeme katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Bariadi na Busega.

“Bodi haijaridhishwa na kasi ya Mkandarasi huyu, kwani amepewa kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 152 vya mkoa wa Simiyu lakini mpaka sasa amesambaza katika vijiji 54 ambayo ni takribani asilimia 30 tu ya kazi anayopaswa kufanya, hivyo tumempa siku 14 aonyeshe mabadiliko la sivyo tutachukua hatua”, amesema Kalolo.

Ameongeza kuwa, tayari Serikali imetimiza jukumu la kutoa malipo kwa Mkandarasi huyo ili kazi ya usambazaji umeme ifanyike, hivyo visingizio vya ucheleweshaji wa kazi havikubaliki na kwa mujibu wa mkataba anapaswa kukamilisha kazi hiyo mwezi Aprili mwaka 2020.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya REA amemuagiza Mkandarasi huyo kutoka kampuni ya Whitecity Guangdong JV, kuwasilisha mpango kazi wake kwa Bodi hiyo, Meneja wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) mkoa wa Simiyu pamoja katika Ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu ili waweze kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa kazi anazofanya.