Waziri Mkuu ahairisha mkutano wa 17 wa Bunge

0
239

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2020/2021 umelenga kutekeleza maeneo ya kipaumbele ikiwa ni pamoja na kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa kuweka mkazo katika upatikanaji wa huduma bora za jamii zikiwemo za Elimu, Maji na Afya.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akiahirisha mkutano wa 17 wa Bunge la 11.

Ametaja maeneo mengine ya kipaumbele kuwa ni ujenzi wa msingi wa uchumi wa Viwanda kwa kuimarisha sekta ya Kilimo kwa kujenga Viwanda vitakavyotumia malighafi inayopatikana nchini, kuimarisha mashirika yanayoendeleza Viwanda na kuanzisha na kuendeleza maeneo ya Viwanda.
 
Waziri Mkuu amewasisitiza Wananchi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo ili kuiwezesha nchi kufikia malengo ya kujenga uchumi imara, unaojitegemea na wenye kuweza kuhimili ushindani.
 
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta zinazogusa Wananchi moja kwa moja na kuhakikisha kuwa matunda ya kukua kwa uchumi yanawafikia Wananchi.
 
“Watanzania wanatakiwa kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli, katika kipindi hiki ambacho amekuwa akichukua hatua za makusudi kuhakikisha anajenga uchumi imara, kuboresha kipato na hali ya maisha ya wananchi”, amesema Waziri Mkuu.

 Bunge limeahirishwa hadi Januari 28 mwaka 2020.