Polisi wa kutuliza ghasia katika mji wa Hong Kong nchini China, wameendelea kupambana na Waandamanaji wanaoendelea na maandamano yao ya kupinga Serikali, huku wakiwa wametanda katika eneo la kati la mji huo.
Mapambano ya leo yamekuwa makali kati ya Waandamanaji na Polisi waliokuwa wakishambuliana kwa wazi, huku Waandamanaji nao wakiendelea kuzuia shughuli za kibiashara kufanyika katika eneo la kati la mji wa Hong Kong.
Jana Serikali ya Hong Kong ilitangaza kuwa, shule zote zitafungwa hii leo kwa sababu za kiusalama, baada ya maandamano hayo kuendelea kuambatana na ghasia.
Mahakama katika mji huo ilitupilia mbali shauri lililowasilishwa na upande wa upinzani, kuwazuia askari kuingia katika maeneo ya vyuo vikuu nchini humo leo, kwa kuwa Wanafunzi watakuwa wakiendelea na mitihani.
